Taarifa ya Serikali kuhusu ugonjwa wa Marburg uliozuka Kagera na namna ya kujikinga 

0
51

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema uchunguzi uliofanyika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa unaojulikana kama ‘Marburg Viral Disease’ katika kata za Maruku na Kanyangereko, Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Akitoa taarifa hiyo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa mtu mmoja  kwenda kwa mwingine au kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu hususani kwa njia ya kugusa majimaji ikiwemo mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au mgonjwa mwenye dalili.

“Hadi sasa serikali yetu imefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi mapya ya ugonjwa huu, hadi sasa ugonjwa haujatoka nje ya eneo lililoripotiwa, kwa hiyo mpaka dakika hii ugonjwa uko katika eneo lililoripotiwa ambako ni mkoani Kagera katika Wilaya ya Bukoba,” amesema Ummy.

Ameongeza kuwa hadi kufikia Machi 21 jumla ya watu nane wamethibitika kuwa na ugonjwa huo, kati yao vifo ni vitano huku wagonjwa watatu wakiendelea na matibabu katika vituo vilivyoandaliwa mkoani humo.

“Dailili za ugonjwa huo ni homa, kuumwa kichwa, maumizvu ya misuli, kuishiwa nguvu, kutapika, kuharisha na kutokwa damu sehemu za wazi za mwili n.k. Ugonjwa huu hauna tiba mahususi isipokuwa kutibiwa kwa dalili alizonazo mgonjwa, kama kuna mtu anaumwa kichwa atatibiwa dalili za kuumwa kichwa,” ameeleza.

Aidha, Serikali imesema inawafuatilia kwa ukaribu watu wote waliotangamana na wagonjwa au wahisiwa ili kudhibiti ugonjwa huo na kuhakikisha hausambai maeneo mengine.