Taarifa ya Simba kuhusu suala la Kagere kusajiliwa Hispania

0
53

Mabingwa wa Tanzania, Klabu ya Simba imesema kuwa haijafanya mawasiliano na Klabu ya Levante UD ya nchini Hispania kuhusu usajili wa mshambuliaji hatari, Meddie Kagere, muite MK 47 (Terminator).

Simba imetoa taarifa hiyo kufuatia uwepo wa taarifa mbalimbali zinazodai kuwa nyota huyo raia wa Rwanda anatarajiwa kutimkia barani Ulaya.

Meneja wa mchezaji huyo, Patrick Gakumba amesema kuwa tayari Levante wameonesha nia ya kutaka kumsajili MK 47, lakini wanataka afanye majaribio kwanza, jambo ambalo meneja huyo anaona halina haja.

Gakumba amesema mchezaji wa kaliba ya Kagere hahitaji majaribio bali anasajiliwa na kuingia uwanjani.

Simba imesema haijafanya mawasiliano kuhusu usajili huo, ambao Gakumba naeleza kuwa Levante imekuwa ikimfuatilia Kagere tangu Simba ilipocheza dhidi ya Sevilla jijini Dar es Salaam, na kupokea kipigo cha magoli 5-4.

“Hakuna yeyote au timu yoyote iliyokuja ikitaka huduma ya Kagere,” amesema afisa wa Simba ambaye hakutaka kutajwa, na kuongeza kuwa kinachosambazwa ni tetesi.

Kagere ambaye sasa yupo nchini Rwanda anaongoza kwa ufungaji wa magoli katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo imesimama kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

Send this to a friend