Taarifa ya TANESCO kuhusu kukosekana huduma ya LUKU nchi nzima

0
67

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema wateja wake watakosa huduma ya mfumo wa ununuzi wa umeme wa malipo kabla ya matumizi (LUKU) usiku wa kuamkia Juni 9 mwa huu kwa muda wa saa mbili ili kufanya maboresho katika kituo cha kujikinga na majanga.

Meneja Mwandamizi wa TEHAMA, Cliff Maregeli amesema kutokana na changamoto hiyo ya kiufundi, wateja wanunue umeme wa ziada ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.

“Siku ya Jumatano usiku kuamkia Alhamisi tutakuwa na shughuli ya kujaribu mifumo yetu ya kuuzia umeme kwa wanunuzi wa LUKU, maboresho haya ni muhimu na yanalenga kuongeza ufanisi kwenye mfumo wa manunuzi ya umeme ili kuhudumia wateja wengi ipasavyo hata pale inapotokea hitilafu ya aina yoyote,” amesema.

Aidha, ameeleza usiku huo watahamishia miundombinu yao ya umeme kutoka kwenye kituo chao kikuu kwenda kwenye kituo cha kujikinga na majanga, na umeme utauzwa kutoka upande huo kupima ufanisi na maendeleo yake.

“Tunategemea kwa muda wa saa mbili kati ya saa 6 hadi saa 8 usiku, wateja hawatakuwa na uwezo wa kununua umeme wakati tukifanya jitihada za kuhama, tutajitahidi kutozidi muda tuliotaja,” ameongeza.

Send this to a friend