Taasisi ya Bill Gates kumtunuku tuzo Rais Samia

0
6

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kupokea tuzo ya ‘The Gates Goalkeepers Award’ iliyoandaliwa na taasisi ya ‘The Gates Foundation’ ya nchini Marekani kwa kutambua mchango wake katika sekta ya afya.

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema Rais Samia ndiye kiongozi wa kwanza kupata tuzo hiyo kwa bara la Afrika, ambapo ni kufuatia ripoti ya utafiti wa demografia na afya ya mwaka 2022 inayoonesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kwa kiwango cha asilimia 80 pamoja na watoto wachanga nchini.

“Taasisi hii imekuwa na utaratibu wa kutoa tuzo mara moja kwa mwaka, lakini tuzo hiyo imekuwa ikitolewa kwa viongozi waliowezesha nchi zao huko wanakotoka kufanikisha au kuwa na mwenendo mzuri wa kuelekea kutekeleza malengo ya kidunia, ya kimataifa endelevu kufikia mwaka 2030,” amesema.

Aidha, amesema tangu kuasisiwa kwa tuzo hiyo, imekwishatolewa mara saba pekee kwa viongozi mashuhuri wachache, huku akiishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga chini ya miaka mitano.