Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini zapewa siku 7 kujieleza

0
52

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa siku saba kwa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kujieleza kwanini zisichukuliwe hatua za kisheria kutokana na kukiuka sheria za nchi.

Katika taarifa ya wizara iliyotolewa Juni 24 mwaka huu imeeleza kuwa THRDC ilitakiwa kuwasilisha orodha na nakala za vyeti vya usajili wa wanachama wake wote, lakini haijafanya hivyo.

Aidha, wizara imesema kuwa taasisi hizo mbili zimeendelea kutekeleza miradi yake mbalimbali bila kuwasilisha taarifa ya fedha wanazopewa na kudhibitishwa na Msajili wa NGOs kama ambavyo sheria inaagiza.

Kwa mujibu wa kifungu namba 13 (b) na (c) cha Kanuni za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali za Mwaka 2018 inataka NGOs kuwasilisha mkataba wa fedha wanazopokea zinazozidi TZS 20 milioni, si zaidi ya siku 10 tangu siku ya kuingia mkataba au makubaliano.

Wizara imeeleza zaidi kuwa THRDC imekuwa ikiratibu kazi mbalimbali za NGOs chini ya mwamvuli ambao haujasajiliwa wa Civil Society Organization Director’s Forum (CDF) kinyume na sheria. Kutokana na hatua hiyo wizara imeiagiza CDF kusitisha shughuli zake zote.

Kwa upande wa LHRC wizara imeeleza kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiratibu shughuli mbalimbali chini ya mwamvuli ambao haujasajiliwa wa Tanzania Civil Society Consortium on Election Observation (TACCEO) kinyume na sheria na hivyo imeagizwa kukoma mara moja.

Kutokana na mapungufu hayo asasi hizo zimepewa hadi Julai 1, 2020 kueleza kwanini zisichukuliwe hatua za kisheria.

Send this to a friend