Wataalamu wa moyo wamesema magonjwa ya moyo yanazidi kuongezeka nchini huku imani potofu zikiendelea kusambaa kuhusu tiba ya magonjwa hayo.
Ameyasema hayo Mkurugenzi wa Tiba katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Tatizo Waane amesema awali walikuwa wakipokea wagonjwa 50 hadi 60, lakini hivi karibuni wagonjwa wamefika 300 hadi 500 kwa siku huku watoto wakiwa 30 hadi 40.
Mambo 4 yatakayomwepusha kijana na shambulio la moyo
“Takwimu zinaonesha karibu asilimia 30 ya vifo duniani vinasababishwa na magonjwa ya moyo. Takwimu za hapa nchini zinaonesha takribani asilimia 30 ya Watanzania wana shinikizo la juu la damu, asilimia 30 wana tatizo la ongezeko la lehemu kwenye damu na asilimia 33 hadi 35 wana uzito uliokithiri na hivyo wako katika hatari ya kupata magonjwa ya moyo,” amesema Dkt. Waane.
Ameongeza kuwa mtindo mbaya wa maisha ukiwemo ulaji mbaya, unywaji pombe, matumizi ya tumbaku na kutofanya mazoezi vinachangia magonjwa ya moyo kwa kiasi kikubwa.