Tahadhari yatolewa kwa wanawake wanaoweka tumbaku sehemu za siri

0
44

Wanawake wanaotumia tumbaku kuweka kwenye sehemu zao za siri ili kupata msisimko wameonywa kutofanya hivyo kwa kuwa wako kwenye hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Akizungumza na Jamhuri, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Saratani kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), Amina Yusuph amesema kitendo hicho ni miongoni mwa sababu za ongezeko la ugonjwa huo katika Kanda ya Ziwa.

“Asilimia 80 ya akina mama wanaokuja kupima saratani ya mlango wa kizazi hukutwa ‘wamepakia’ tumbaku ukeni. Kitendo hiki si sahihi na ni hatari,” amesema.

Daktari amesema wanapoulizwa sababu za kufanya hivyo hujibu kwamba hiyo ni moja ya njia ya kuwafanya wapate msisimiko na kumaliza haja zao za kimwili.

Mbali na hayo, sababu nyingine zilizotajwa zinazochangia ugonjwa huo ni pamoja na kuzaa watoto wengi bila kupishana, kuwa na wapenzi wengi, walioanza mapenzi na kuzaa katika umri mdogo pamoja na walioathiriwa na magonjwa ya zinaa.

Aidha, ameongeza kuwa ugonjwa huo huchukua maisha ya wanawake wengi hivyo ni vyema kujiwekea utaratibu wa kupima afya zao mapema na kupewa matibabu ya kuongeza siku hata kama wamechelewa kuliko kukaa nyumbani.

Send this to a friend