Takwimu: umaarufu wa Haji Manara katika mtandao wa Instagram waporomoka

0
51

Agosti 24 mwaka huu habari kubwa iliyogonga vichwa vya habari katika sekta ya michezo ni ‘usajili’ wa Haji Manara kwenda Yanga, zikiwa ni siku chache tu tangu alipoachana na klabu ya Simba aliyokuwa nayo kama msemaji wake kwa miaka 6, kuanzia mwaka 2015.

Tukio hili lilivuta hisia za wengi kwani ni ukweli usio na shaka kwamba ushabiki wa Simba na Yanga ni moja ya sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania walio wengi na wakati mwingine ushabiki wa timu hivi umekuwa hadi wa kuzaliwa. Unazaliwa baba Yanga basi na mtoto unaishia kuwa Yanga, na Simba vivyo hivyo.

Habari zilikuwa nyingi kwenye redio, magazeti na televisheni na uchambuzi na maoni ya kila namna lakini pengine eneo ambalo mjadala huu ulikuwa mkubwa zaidi ni kwenye mitandao ya kijamii. Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha kwamba Tanzania ina watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 29 huku asilimia kubwa wakiwa kwenye mitandao ya kijamii hivyo basi imeendelea kuwa sehemu muhimu sana ya mijadala ya kila siku kwenye burudani, siasa, michezo na kadhalika.

Moja ya kipimo cha umaarufu wa mtu kama Hajji Manara ambaye kazi yake inamtaka kuzungumza na kuwasiliana na watu kwa kiasi kikubwa ni idadi ya watu wanaomfuatilia kwenye mitandao ya kijamii. Hapo jana, Septemba 9 2021 katika akaunti yake ya Instagram Manara aliposti ujumbe ufuato akisema kuwa tangu ahamie Yanga idadi ya watu wanaomfuatilia imeongezeka. Hata hivyo wachambuzi wa mitandao ya kijamii na ushawishi wake kwenye michezo na biashara wanasema Hajji haelewi maana ya takwimu hizo alizoposti kwani kiuhalisia zinaonesha ameshuka katika nguvu yake ya ushawishi kwenye mitandao ya kijamii. Ufuatao ni uchambuzi wa takwimu hizo alizopost na kwa nini maana yake ni kushuka na si kupanda kama alivyoeleza Manara.

Post ya Manara

Impressions: hii maana yake ni mara ngapi watu wameona posts zote ulizoposti katika akaunti yako katika kipindi fulani (saa, siku, wiki, mwezi au mwaka). Maana yake kama mtu mmoja ameona posti yako moja mara 3 hiyo ni impression ila kiuhalisia idadi ya watu walioona ni mtu mmoja tu.

Profile visits: Hii sasa ni idadi ya watu halisi ambao wameona akaunti yako. Maana yake kama una posti nane, mtu mmoja akaziona kila posti mara moja moja hizo tunaita impressions ila yule mtu mmoja aliyeziona tunamuita profile visit au kwa lugha ya kitaalamu “unique account.”

Sasa turudi kwenye namba alizoposti Manara

⦁ Anasema kapata wastani wa watu milioni 17 kati ya siku 4 hadi tano. Sahihisho: hawa si watu, ni impressions maana yake mara ambazo watu wameona posti zote alizoposti katika wiki ya Agosti 26 hadi Septemba 1. Hizi ni siku 7 na si 4 au 5 kama anavyosema. Wastani wa impressions zake kwa wiki hiyo ni 2,411,031 kwa siku. Chini ya impressions hizo za Manara ambazo ni 16,877,222 kwa wiki kuna numba -37.5% (maana ya alama ya kutoa au hasi ni anguko). Ingekuwa ongezeko ingekuwa alama ya kujumlisha (+) au chanya. Maana yake impressions za Manara zimeanguka kwa asilimia 37.5 na si kwamba zimeongezeka kwa asilimia 37.5.

⦁ Katika sehemu ya pili ya profile visits za Manara kuna namba 594,926 hii sasa ndiyo idadi ya watu ambao wameona hizo posti za Manara kwa wiki nzima ambayo ukitaka kujua wastani wa mtu mmoja ameona posti mara ngapi unachukua idadi ya impressions unagawanya kwa idadi ya profile visists maana yake 16,877,222 gawanya kwa 594,926 unapata kama 3 hivi. Maana yake katika watu hao 594,926 walau kila mmoja katika kipindi cha wiki moja ameona posti za Manara Instagram walau posti 3. Kwenye akaunti yake Manara chini ya ile 594,926 kwa wiki kuna namba -51.4% (maana ya alama ya kutoa au hasi ni anguko). Ingekuwa ongezeko ingekuwa alama ya kujumlisha (+) au chanya. Maana yake idadi ya watu wanaotazama nini Manara anaposti Instagram imeanguka kwa asilimia 51.4 (zaidi ya nusu) na si kwamba imeongezeka kwa asilimia 51.4.

Ongezeko huoneshwa kwa alama ya chanya na inakuwa na rangi ya kijani (tazama chini), anguko huoneshwa kwa alama ya hasi.

Sababu ambazo huenda zimechangia hali hii ya kushuka kwa umaarufu wa Manara katika mtandao wa Instagam:

⦁ Utafiti unaonesha kwamba Simba ina mashabiki wengi zaidi katika mitandao ya kijamii kuliko Yanga na imejipanga na kuwekeza zaidi katika eneo hilo ukitazama idadi ya akaunti zake rasmi (verified), idadi ya wafuasi katika akaunti hizo na idadi ya posti na engagement (ushiriki wa washabiki kwenye comments, shares, etc) ya mashabiki kwa siku.

⦁ Kupotea kwa imani ya mashabiki kuhusu ushawishi wa Manara baada ya kuhamia Yanga. Imani hii yawezekana imepotea kwa baadhi ya mashabiki wa pande zote mbili, wale wa Simba wakiona wamesalitiwa na wale wa Yanga wakiwa bado na wasiwasi kama kweli hatawaacha na kwenda timu nyingine. Hii inadhihirika kwa namba ambavyo watu wamekuwa wakisambaza clips zake akiapa kwamba yeye ni Simba na Simba na timu bora na hizi za sasa akisema yeye ni Yanga na Yanga ni timu bora (Ushawishi unahitaji msimamo usioyumba).

Nini maana ya mwenendo huu wa Manara katika mitandao ya kijamii?

⦁ Atalazimika kutafakari na kupata ushauri wa wataalamu wa mawasiliano na ushawishi ili kujenga mkakati mpya wa kukua kwenye mitandao hiyo.

⦁ Iko hatari ya makampuni ya kibiashara kama yakifanya uchambuzi wa kisayansi kumpunguzia idadi ya matangazo au bei ambazo wanamlipa kwa tangazo moja au kufuta kabisa mahusiano ya kibiashara kwani namba hizi hutumika sana kwenye kuamua kuhusu ushawishi (inflencing hasa kwenye mitandao ya kijamii).

__
Mwandishi wa Makala hii amejitambulisha kwa jina la Kifani Mjanenga, Mchambuzi wa Mifumo ya Mawasiliano na Mitandao ya Kijamii, anapatikana kwa barua pepe mjanenga@protonmail.com

Send this to a friend