Takwimu: Wanaume waongoza kuua wake zao Tanzania

0
50

Jumla ya matukio 908 ya ya wanandoa kuuana na kujiua wenyewe yameripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini tangu mwaka 2019 hadi Septemba 30 mwaka huu.

Takwimu zilizotolewa na jeshi la polisi zinaonesha kuwa katika matukio hayo, wanaume 750 wameua wake zao na 74 kati yao wamejiua huku wanawake 158 wakiua waume zao na 39 kati yao kujiua.

Katika mahojiano na gazeti la HabariLEO, Msemaji wa Jeshi la Polisi, SACP David Misime amewataka wananchi kuanzia ngazi ya familia hadi viongozi wa dini kuendelea kutoa tahadhari na mafundisho ili kupunguza matukio hayo kwani yanasababisha madhara yakiwamo watoto yatima.

Mchanganuo wa matukio hayo kwa mwaka 2019 unaonesha kuwa waume walioua wake zao ni 328 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 28. Wanawake walioua waume zao ni 58 na kati yao 18 walijiua baada ya kuua waume zao.

Mwaka 2020 waume walioua wake zao ni 226 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 30, huku wanawake walioua waume zao ni 71 na kati yao 12 walijiua baada ya kuua waume zao.

Mwaka 2021 (hadi Septemba 30) waume walioua wake zao ni 156 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 16, huku wanawake walioua waume zao ni 29 na kati yao 9 walijiua baada ya kuua waume zao.

Idadi kubwa ya matukio hayo imeelezwa kuchagizwa na watu kushindwa kumudu sonona na msongo wa mawazo, hasa kutokana na hali ya uchumi inayopelekea wanaume kuanza kuhisi mambo yasiyokuwepo.

“Anaanza kuhisi kwamba haheshimiki na pia anahisi kwamba kuna mwanaume ‘anamsaidia’ kwa mkewe hivyo, hata mwanamke akitoka kidogo tu, anadhani ‘amekwenda’,” amesema Englibert Kiondo, mwanasaikolojia na muelimishaji wa jeshi la polisi akizungumza na gazeti hilo.

Kuondoa tatizo hilo wanandoa na wananchi wametakiwa kuwa na utamaduni wa kuwashirikisha wana jamii mambo yanayowatatiza ili wayatafutie ufumbuzi .

Send this to a friend