TAMNOA: Punguzo la tozo larejesha ukuaji wa matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu

0
37

DAR ES SALAAM, SEPTEMBA 8, 2022.

Umoja wa waendesha huduma za simu za mikononi (TAMNOA) umebainisha kuwa kutokana na tozo za miamala ya simu zilizoanza mwaka 2021 mwezi Julai, na kwa kuangalia mlolongo wa matukio tangu kuanzishwa kwa tozo hizi, pamoja na kupungua kwa matumizi ya huduma za kifedha, hali ya mwaka huu wa fedha ni ya kuridhisha.

Taarifa iliyotolewa na TAMNOA kwa vyombo vya habari imesema hali hii ya kuridhisha imetokana na mazungumzo ya kina baina ya watoa huduma, wadau na serikali tangu tozo hizo zilizolenga kuongeza kasi ya ufikishwaji wa huduma kwa jamii zilipoanza mwaka jana. Mazungumzo hayo yalipelekea punguzo la hadi asilimia 60 hadi sasa, ambapo asilimia 30 ilipunguzwa kwenye hatua ya mwanzoni hadi kufikia asilimia 70 mnamo mwezi wa tisa mwaka jana mara tu baada ya tozo hizo kuanza. Baada ya punguzo hilo mwenendo wa kurudi wigoni kwa wateja ulianza kuonekana.

Punguzo la pili lilifanyika kwenye mwaka huu wa fedha wa serikali 2022, ambapo asilimia 43 ilipunguzwa kutoka kwenye asilimia 70 iliyosalia, sawa na asilimia 30 ya kiwango cha mwanzo, hivyo kufikia jumla ya punguzo la asilimia 60.

Hatua hii ya serikali kupunguza tozo kwa kiasi hiki kikubwa imeendelea kudhihirisha uwepo wa mandhari shirikishi kati ya watoa huduma na serikali pale changamoto zinapojitokeza.

“Kwa sasa muonekano wa kibiashara unaendelea kuwa wenye hali nzuri na tunategemea kuendelea kushirikiana na serikali kukuza sekta na kufikisha huduma zake jumuishi kwa watanzania”, imesema taarifa iliyotolewa na TAMNOA.

Send this to a friend