TANESCO: Ongezeko la kodi ya majengo kwenye LUKU ni madeni ya nyuma

0
112

Kufuatia malalamiko kuhusu ongezeko la viwango vya malipo ya kodi ya majengo katika ununuzi ya umeme kuanzia Julai 1, 2024, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema hakuna ongezeko lolote llililofanyika kwenye viwango vya kodi ya majengo nchini isipokuwa ni madeni ya nyuma yaliyotakiwa kulipwa mwaka wa fedha 2023/24.

TANESCO imesema Julai 26, 2023 yalitangazwa mabadiliko ya viwango vya kodi ya majengo vilivyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka shilingi 1,000 hadi 1,500 kwa nyumba zisizo za ghorofa, na kutoka shilingi 5,000 hadi 7,500 kwa nyumba za ghorofa.

“Hii inamaanisha kwa mteja aliyenunua umeme kati ya tarehe 1 hadi 25 Julai 2023 (kabla ya mabadiliko ya viwango vya kodi kuanza) alilipa kiwango cha zamani, yaani shilingi 1,000 na hivyo kuwa na baki ya deni la shilingi 500 ambayo alitakiwa kulipa, na mteja aliyelipia shilingi 5,000 ya zamani alitakiwa kuwapa shilingi 7,500 hivyo kuwa na baki ya deni la shilingi 2,500. Hii pia ni kwa wale ambao ndani ya kipindi hicho walilipa kodi ya jengo kwa mkupuo.

“Baada ya hapo mteja ataendelea kulipia viwango vya kawaida kulingana na aina ya nyumba anayoishi kama mwongozo wa TRA wa tarehe 26, Julai 2023 unavyoelekeza yaani shilingi 1,500 kwa nyumba ambayo siyo ghorofa na shilingi 7,500 kwa safu moja ya nyumba ya ghorofa kila mwezi,” imeeleza TANESCO.

Mbali na hayo TANESCO imewatoa wasiwasi wateja wake na kuwahimiza kuendelea kununua huduma ya umeme, na iwapo watahitaji kuangalia madeni ya kodi ya majengo wanaweza kufanya hivyo kwa kupitia mfumo wa Nikonekt au kutembelea ofisi za Halmashauri za Manispaa (TAMISEMI) zilizo karibu.

Send this to a friend