Tanzania inaendelea kukabiliana na virusi vya corona- Dkt. Abbasi
Serikali ya Tanzania imetupilia mbali shutuma kwamba imekuwa haichukui hatua madhubuti kukabiliana na mlipuko wa virusi vya corona.
Akizungumza na BBC, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa maabara ya taifa imefungwa na zoezi la upimaji limesitishwa kutokana na uchunguzi unaoendelea juu ya vifaa vya upimaji wa virusi hivyo.
Licha ya hatua hiyo, Dkt Abbasi amesema kuwa waathirika wa homa ya mapafu (COVID-19) wanaendela kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.
“Sio kweli kwamba hatuendelei na mapambano dhidi ya COVID-19 nchini, hapana. Watanzania wengi wanaendelea na maisha yao kama kawaida, na tayari tulishashema kama mtu ana dalili afike katika kituo cha afya,” Dkt, Abbasi ameiambia BBC.
Kauli ya serikali inakuja ikiwa ni siku moja tangu Ubalozi wa Marekani nchini ulipotoa tahadhari kuhusu janga hilo, huku ukiwataka watu kuchukua tahadhari.
Licha ya serikali kutokuchukua hatua kali kukabiliana na corona kama yalivyofanya mataifa mengine, baadhi ya wananchi wameendelea kujikinga kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, pamoja na kuepuka mikusanyiko.