
Tanzania imeihakikishia Jumuiya ya Kimataifa inayojihusisha na ufuatiliaji na udhibiti wa utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuboresha mifumo yake ya udhibiti wa vitendo hivyo nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi. Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Ubadilishaji wa Taarifa za Udhibiti wa Fedha Haramu Duniani (EGMONT Group meeting), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kujenga mfumo imara wa kupambana na uhalifu wa kifedha, ikiwa ni pamoja na kuimarisha taasisi za udhibiti na ushirikiano wa kimataifa, hatua ambayo imewezesha Tanzania kuondolewa kwenye orodha ya nchi zenye mapungufu katika udhibiti wa utakasishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, baada ya kutekeleza kwa mafanikio mpango wa hatua uliowekwa na Kikosi Kazi cha Kudhibiti Utakatishaji Fedha (FATF).
“Uamuzi wa Umoja wa Ulaya kuiondoa Tanzania kwenye orodha ya nchi zenye hatari kubwa umefungua ukurasa mpya wa uaminifu wa kifedha na kuvutia uwekezaji wa kigeni na tunajivunia mafanikio haya ambayo ni matokeo ya uongozi thabiti, mageuzi ya kisheria, na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zetu za ndani na washirika wa maendeleo,” amesema Mhandisi Munde.
Amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi wanachama wa Kikundi cha EGMONT na makundi mengine kama Kikundi cha Afrika Mashariki na Kusini cha Kuzuia Utakasishaji Fedha – ESAAMLG, ili kuhakikisha mifumo ya ndani inalingana na viwango vya kimataifa vya uadilifu wa kifedha.







