Tanzania kunufaika na mkutano wa utalii

0
49

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana amesema Tanzania  inatarajia kunufaika  na fursa mbalimbali zitakazotokana na Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani [UNWTO-CAF] utakaofanyika jijini Arusha kuanzia Oktoba 5 hadi 7, mwaka huu.

Ameyasema hayo katika mkutano na vyombo vya habari jijini Arusha alipokuwa akieleza kuhusu kufanyika kwa mkutano huo ambao mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, amesema mkutano huo utainufaisha Tanzania kwa kukuza na kuendeleza utalii, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na lengo litakalowekwa la haki ya msingi ya binadamu kutembelea sehemu mbalimbali ya vivutio vya utalii bila vikwazo vyovyote.

“Mkutano huu utahusisha matukio mbalimbali ukiwemo mkutano wa mawaziri wa utalii kutoka nchi wanachama, jukwaa la uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na mafunzo kwa wadau wa sekta ya utaliii yaani Marketing Symposium kwa lengo la  kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu kutangaza utalii” amesema.

Chana ametoa rai kwa wadau wote wa utalii hususani wakazi wa jiji la Arusha na maeneo ya jirani wanaotoa huduma za malazi, mawakala wa biashara za utalii na waongoza watalii kuonesha ukarimu wa hali ya juu kwa washiriki wa mkutano katika kipindi chote watakachokuwa nchini.

Send this to a friend