Tanzania kununua ARVs kutoka Uganda

0
20

Tanzania inatrajia kuanza kununua dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI (ARVs) kutoka Uganda.

Hayo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya serikali za pande zote mbili, ambapo makubalino mengine ni kufunguliwa upya kwa njia ya Mwanza – Port Bell Kampala, ambayo hapo awali ilikuwa haifanyi kazi lakini hivi sasa inafanya kazi.

Kwa sasa njia hiyo imepunguza kwa kiwango kikubwa muda wake wa mpito ambapo sasa huchukua siku 4 tu tofauti na siku 9 hapo awali, hivyo kupunguza gharama za kufanya biashara.

Aidha, Rais wa Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Ushirikano (MoU) mbili Ikulu Entebbe nchini Uganda.

Hati hizo ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa 400KV kutoka Masaka – Mutukula – Nyakanazi – Mwanza na nyingine ni kuhusu ushirikiano wa masuala ya Ulinzi na Usalama baina ya nchi hizo mbili.

Wakati huo huo, Tanzania imekubali kupunguza gharama za usafirishaji ambapo kwa sasa Uganda italipa Dola za Kimarekani 10 kwa lori litakalopita kila kilomita 100 katika njia ya kutoka Mutukula hadi Dar es Salaam kuanzia mwaka mpya wa fedha Julai mosi mwaka huu.

Pia, Uganda imeahidi kutuma tani nyingine elfu 10 za sukari ili kufidia upungufu wa bidhaa hiyo Tanzania.

Utiaji saini huo ulishuhudiwa pia na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambapo amesisitiza kuendelea kushirikiana kwenye utengenezaji wa chanjo na dawa za binadamu na mifugo.

Send this to a friend