Tanzania kupokea Watalii wengi kutoka Urusi

0
41

Ule msemo usemao ‘vita vya panzi furaha ya kunguru’ umejidhihirisha ambapo Tanzania inatarajia kupata watalii wengi siku za hivi karibuni kutokea Urusi kutokana na nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Marekani.

Hayo yamebainishwa katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Fredrick Kibuta na Mbunge kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi, Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi.

“Kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Urusi, watalii wengi raia wa Urusi wanatarajiwa kuja Afrika ikiwemo Tanzania na kwamba Tanzania iandae mazingira wezeshi ikiwemo kuzingatia suala la usalama wa watalii”, alieleza Revaldovich.

Mbunge huyo alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Serikali ya Urusi kukuza uhusiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuanzisha uhusiano wa kimiji (sister City) na kutolea mfano jimbo la Skha-Yakutia linaweza kuanzisha uhusiano na mkoa wa Arusha au Kilimanjaro ambayo ni mikoa ya Utalii kama ilivyo kwa jimbo hilo.

Hata hivyo, Kiongozi huyo aliwakaribisha watalii raia wa Tanzania kutembelea jimbo lake la Sakha-Yakutia ambalo kwa miaka minne iliyopita imekuwa likipokea watalii wengi kutoka barani Afrika na nchi nyingine duniani. Watalii wanapenda kutembelea jimbo hilo kwa ajili ya kuogelea kwenye maji yenye nyuzi joto hasi sitini na moja (-61 nyuzi joto).

Kwa upande wake, Kibuta aliihakikishia Urusi kuwa Tanzania ipo tayari kupokea watalii kutoka nchi hiyo na kwamba hali ya hewa ni nzuri na usalama kwa watalii upo.

Ameongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa miundombinu ya kuridhisha ya utalii nchini, Serikali inaendelea kuwekeza na kuboresha kwenye miundombinu hiyo.

Send this to a friend