Tanzania kurekebisha sheria inayoruhusu Wananchi, NGOs kuishtaka katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika

0
38

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International uamuzi wa Tanzania kuondoa itifaki au kipengele ambacho kinaruhusu wananchi na asasi za kiraia kuishtaki katika Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu ya Afrika kunahatarisha hali ya haki za binadamu.

Katika taarifa yake, shirika limesema uamuzi huo utawanyima wananchi na mashirika hayo kupata haki.

“Hatua hiyo inawazuia wananchi na mashirika yaliyo ndani ya nchi kwenda moja kwa moja katika mahakama hiyo kuishtaki serikali kuhusiana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, jambo ambalo linaashiria kuwa serikali inakwepa kuwajibishwa,” Japhet Biegon, muwakilishi wa Amnesty International Afrika amesema.

Tanzania ambayo ndiyo mwenye wa mahakama hiyo yenye ofisi zake jijini Arusha itakuwa nchi ya pili kuondoa itifaki hiyo baada ya Rwanda.

Katika barua yake kwenda Umoja wa Afrika, ambao nchi wanachama wake ndio wameanzisha mahakama hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi imesema kuwa inaondoa itifaki hiyo kwa sababu mahakama imeshindwa kutekeleza baadhi ya mambo ambayo nchi iliainisha kuhusu kuruhusu wananchi na asasi za kiraia kuishtaki.

Mwaka 2010 Tanzania ilitoa azimio katika mahakama hiyo kuwa wananchi na mashirika ya kiraia yataweza kuishtaki katika mahakama hiyo pale tu ambapo suala hilo limeshapitia kwenye mahakama zote au taratibu nyingine za kisheria za ndani.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema Tanzania ilituma maombi ya kuondolewa itifaki hiyo ambayo inapingana na sheria ya Tanzania na kusisitiza kuwa kwa sasa haijajitoa katika mahakama hiyo, bali inasubiri marekebisho hayo.

“Tunachosubiri kwa sasa ni marekebisho hayo ila ikishindikana basi tutajitoa. Kwa sasa bado hatujajitoa kama inavyosemekana,” alisema.

Takribani 40% ya kesi zote zilizofunguliwa katika mahakama hiyo yenye wanachama 52, zimefunguliwa dhidi ya Tanzania.

Hata hivyo mpaka sasa nchi tisa kati ya 30 zilizoridhia itifaki hiyo zimesaini kuwapa uhuru huo wananchi wake kudai haki zao mahakamani pindi Serikali inapowatendea kinyume. Zilizosaini ni Benin, Burkina Faso, Ivory Coast, Gambia, Ghana, Mali, Malawi, Tanzania na Tunisia.

Send this to a friend