Tanzania kushika nafasi ya Ukurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika

0
44

Tanzania inatarajia kushika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji mbadala (Alternative Executive Director) katika Kundi la Magavana wa Afrika Mashariki katika Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuanzia mwezi Agosti, mwaka huu.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.) wakati wa Mkutano wa kawaida wa Magavana wa Kundi la Nchi za Afrika Mashariki ambao ni wanachama wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ikiwa ni maandalizi ya mikutano ya mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki hiyo inayofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.

Dkt. Mwamba ameeleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika imeweka utaratibu wa mzunguko wa uongozi katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ambao ni Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri na kwa upande wa Tanzania kunakuwa na Mkurugenzi Mtendaji mbadala.

‘’Katika mkutano huu tumezungumzia pia mzunguko wa viongozi ambao ni Mkurugenzi Mtendaji na Mshauri na sisi Tanzania kuanzia mwezi Agosti, 2024 tutashika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji Mbadala katika Benki hiyo ambaye atakuwa anachukua nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji anapokuwa anapata udhuru’’ amesema Dkt. Mwamba.

Aidha, Dkt. Mwamba ameeleza kuwa mkutano huo ulijadili kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ambayo hivi karibuni yamekuwa yakisababisha maafa mbalimbali na kukubaliana kuanzishwa kwa mfuko wa maafa ambao utakuwa unasaidia nchi zitakazo athirika na mabadiliko hayo ikiwemo mvua zisizotarajiwa za El nino.

Mkutano wa Kundi la Nchi za Afrika Mashariki ambao umeshirikisha Wajumbe kutoka nchi tisa (9) ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Somalia, South Sudan, Eritrea na Seychelles, ni utangulizi wa Mkutano wa 59 wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika Nairobi, Kenya.

Send this to a friend