Serikali imesema inaendelea kushirikiana na Serikali ya Burundi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kuwarejesha kwa hiari yao wakimbizi kutoka nchi ya Burundi waliopo Tanzania kama sehemu ya jitihada za kusaidia kurejesha maisha ya kawaida kwa wakimbizi hao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo katika Mkutano wa 25 wa Pande Tatu Kuhusu Urejeshaji wa Hiari wa Wakimbizi Kutoka nchini Burundi wanaohifadhiwa Tanzania uliofanyika jijini Bujumbura .
“Ni jukumu letu kusaidia wakimbizi kurudi nyumbani kwa heshima na usalama. Tutaendelea na juhudi za kuwahamasisha, huku tukishirikiana kwa karibu na pande zote husika,” Amesema Sillo.
Aidha, Serikali ya Tanzania imependekeza kwa Serikali ya Burundi kuanzisha maeneo tengefu ambapo miundombinu ya huduma za kijamii zitaboreshwa zaidi katika maeneo hayo ili kutoa motisha zaidi kwa wakimbizi kurejea nyumbani.
Hata hivyo, Sillo alieleza kuwa Serikali ya Tanzania haifurahishwi na na kasi ya urejeaji licha ya jitihada kubwa sana zilizofanyika za uhamasishaji, jambo ambalo linatulazimu kuwa wabunifu zaidi na kufikiria njia mbadala ili kuhakikisha wakimbizi walioko wanapata suluhisho la kudumu.