Tanzania kutokomeza VVU/UKIMWI ifikapo 2030

0
65

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza TACAIDS na Wizara ya Afya kwa kushirikiana  na wadau wote wa mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI/UKIMWI kuweka mikakati ya kutokomeza ubaguzi na unyanyapaa kwa watu waishio na maambukizi, ikiwa ni moja ya malengo ya kutokomeza ifikapo mwaka 2030.

Ameyasema hayo leo Desemba 1, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Lindi ambayo yamekwenda na kaulimbiu inayosema “Imarisha Usawa.”

Rais ameeleza kuwa kukosekana kwa usawa kunarudisha nyuma juhudi za Tanzania kufukia lengo la kutokomeza VVU/UKIMWI, hivyo ameagiza maadhimisho hayo yatumike kuweka mikakati itakayoimarisha usawa.

Kenya yakumbwa na uhaba wa kondomu

Aidha amesisitiza kuwa maambukizi yanayokua kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 24 yanapaswa kuzuiliwa ikiwemo kuelekeza nguvu nyingi kutoa elimu kwa jamii ili kusimamisha maambukizi hayo.

“Kwa mwendo ule ulioelezwa kwenye ripoti tofauti hapa, kwamba kuna maambukizi yanakua ya vijana wetu wa miaka 15 hadi 24 tusipozuia lile safari yetu itakuwa ndefu sana ya kutokomeza balaa hili,”amesisitiza.

Lengo la kimataifa ambalo Tanzania pia inatekeleza ni kumaliza VVU na UKIMWI (malengo ya sifuri tatu) ifikapo mwaka 2030; yaani sifuri ya kwanza ni kusiwe na maambukizi mapya ya VVU, sifuri ya pili kusiwe na vifo vitokanavyo na UKIMWI na sifuri ya tatu kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU.

Send this to a friend