Tanzania kuwa Kitovu cha uzalishaji, uchakataji na usafirishaji wa madini

0
66

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imefikia uamuzi wake wa kuingia makubaliano na kampuni zenye uwezo wa kuchimba na kuchakata madini nchini ili nchi iweze kunufaika na kupata faida kutokana na raslimali hizo kwa kuunda kampuni za ubia na hivyo Serikali kunufaika kupitia tozo, kodi, ajira, maendeleo ya miundombinu na ukuaji wa teknolojia.

Akishuhudia utiaji saini wa mkataba mkubwa na wa kati baina ya Serikali ya Tanzania na Kampuni tatu za uchimbaji madini kutoka nchini Australia amesema mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini kinywe na Mkoa wa Songwe uko katika ukanda wenye madini adimu ndio maana miradi iliyowekwa saini iko katika Wilaya za Lindi, Ulanga na Songwe.

“Utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulianza tangu mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbali ambapo hadi sasa kuna kiasi cha tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika kijiji cha Chilalo ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18, tani milioni 63 zenye wastani wa asilimia 7.6 yaliyogundulika katika kijiji cha Epanko nayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 18, tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.8 zenye madini adimu yamegundulika katika kijiji cha Ngwala ambayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20,” amesema Rais Samia.

Mbunge: Misafara ya viongozi inakwamisha shughuli za wananchi

Ameongeza kuwa kufuatia uwepo wa madini hayo nchini, wawekezaji wakubwa duniani wameonesha kuvutiwa na Tanzania na hivi karibuni wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Marekani nchini, Kamala Harris walizungumzia umuhimu wa madini hayo pamoja na mradi wa Nikeli wa Kabanga na kiwanda cha usafishaji madini kitakachojengwa Kahama.

Rais Samia alisisitiza “Katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini haya na hivyo kuvutia uwekezaji mahiri, vilevile kwa kutumia nafasi yetu kijiografia ambayo tumezungukwa na nchi nane ambazo baadhi zina madini kama haya fursa hiyo itatufanya Tanzania kuzidi kutunufaisha hasa kwa kuwa tutakuwa na viwanda vya kuchakata madini hayo hapa lakini pia tuna njia za kuaminika za kusafirisha madini hayo.”

Naye Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema miradi hiyo ya madini ni kielelezo tosha kuwa Rais Samia ameamua kwa dhati kuisimamia sekta ya madini na hivyo ukuaji wa sekta ya madini katika mchango wa Pato la taifa umeongezeka zaidi katika kipindi kifupi ambapo Julai hadi Septemba 2022 sekta ya madini imeshachangia asilimia 9.7 ikiwa ni asilimia 0.3 kufikia lengo lililowekwa katika malengo ya Taifa.

Send this to a friend