Tanzania kuwa mwenyeji Tuzo za Dunia za Utalii WTA

0
4

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Tuzo za Dunia za Utalii (World Travel Awards – WTA) kwa Afrika na Kanda ya Bahari ya Hindi kwa mara ya kwanza Juni 28, mwaka huu ambapo wageni zaidi ya 500 kutoka kote duniani wanatarajiwa kuhudhuria.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru amesema taasisi na mashirika 50 ya Tanzania yakiwemo 38 kutoka sekta binafsi na 12 kutoka taasisi za serikali watagombea tuzo hizo na na nchi nyingine katika sekta ya utalii barani Afrika.

“Hizi ni tuzo kubwa zaidi za utalii katika kanda yetu, na Tanzania imepata heshima kubwa kuziandaa,” amesema Mafuru na kuongeza kuwa “Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika itakayokuwa mwenyeji wa tukio la WTA kwa mwaka huu. Hafla nyingine zitafanyika Mexico, Hong Kong, Italia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).”

Aidha, Mafuru amesema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kwa mwaka huu kutokana na ushahidi wa kukua kwa mafanikio na sifa yake katika sekta ya utalii.

Ameongeza kuwa tukio hilo litatumika kutangaza vivutio mbalimbali vya Tanzania, kama vile safari za wanyamapori, urithi wa kitamaduni, utalii wa fukwe na michezo