Tanzania kuwa nchi yenye miradi mingi ya Benki ya Dunia

0
21

Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Mara Warwick amesema kwa sasa benki hiyo imeidhinisha miradi yenye thamani ya USD bilioni 4.9 (sawa na shilingi trilioni 11.2) na inaelekea kuongeza miradi mingine 5 yenye thamani ya USD bilioni 1.15 (sawa na shilingi trilioni 2.6).

Ameongeza kuwa mwaka ujao itaongeza zaidi hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye miradi mingi na muhimu inayofadhiliwa na benki hiyo.

Warwick amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Rais Samia ameiomba Benki ya Dunia kuendelea kushirikiana na Tanzania (Bara na Zanzibar) katika kujenga uchumi utakaoyagusa makundi yote ya jamii hususani kuwafikia watu masikini, kuboresha huduma za kijamii hususani elimu na afya, kuimarisha miundombinu, kuwawezesha wanawake kiuchumi ambao wamebeba majukumu makubwa ya familia, na kujenga mifumo ya kidijiti itakayorahisisha utendaji kazi ikiwemo ukusanyaji wa mapato.

Kwa upande wake Warwick ameongeza kuwa benki hiyo itaendelea kujikita kuwasaidia watu masikini na watu waishio katika mazingira hatarishi kwa kuhakikisha inashiriki kuimarisha miundombinu, masoko, elimu ya msingi, sekondari na vyuo, kuweka mifumo ya kidijiti na kwa Zanzibar kusaidia katika mradi wa nishati ya umeme na uboreshaji wa miji na vijiji.

Send this to a friend