Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa wameeleza azma yao ya kuimarisha uhusiano uliopo wa kisiasa na kiuchumi baina ya nchi hizo mbili wanachama wa SADC pamoja na kuimarisha Tume ya pamoja (BNC).
Akizungumza katika Ofisi za Majengo ya Muungano, Pretoria nchini Afrika Kusini Rais Samia amesema kikao cha pili cha BNC kimeziwezesha nchi zote mbili kukubaliana kuhusu njia zaidi za ushirikiano ikiwemo kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya biashara na uwekezaji.
“Kwa watu wa Afrika Kusini na Tanzania hii inamaanisha biashara zaidi, fursa zaidi za uwekezaji, uhamisho zaidi wa teknolojia, fursa zaidi za elimu na mwingiliano zaidi wa kitamaduni,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa ziara yake nchini humo itaimarisha zaidi uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili na kufungua fursa mpya za kibiashara na uwekezaji huku akiwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwa rafiki na mshirika wa kuaminika kwa Serikali na watu wa Afrika Kusini.
Ziara ya Rais Samia nchini SA inaenda sambamba na kikao cha pili cha Tume ya Pamoja ya Afrika Kusini na Tanzania ambapo nchi hizo mbili zilikagua utekelezaji wa kikao cha kwanza cha BNC kilichofanyika jijini Dar es Salaam Mei, 2017 ambapo zilijadili masuala kadhaa ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja yakiwemo uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa amani na usalama.