Tanzania na Angola kuimarisha ushirikiano katika biashara na uwekezaji

0
11

Serikali ya Tanzania imetangaza kuondoa masharti ya viza za utalii kwa raia wa Angola wanaotaka kutembelea nchi hiyo, hatua inayolenga kurahisisha safari, biashara, na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Tangazo hilo limetolewa leo na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wake na Rais wa Angola, João Lourenço, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Kiserikali ya siku tatu.

Rais Samia amesema kuwa uamuzi huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Angola na kuhimiza ushirikiano wa kibiashara. “Hatua hii itarahisisha safari za wananchi wa mataifa yetu mawili na kufungua fursa zaidi katika sekta za biashara na uwekezaji,” alisema Rais Samia.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamesisitiza umuhimu wa kuhamasisha biashara na uwekezaji, wakihimiza wafanyabiashara wa Tanzania na Angola kutumia fursa zinazotolewa na Eneo Huru la Biashara la SADC na AfCFTA ili kuongeza ushirikiano wa kiuchumi.

Aidha, makubaliano (MOU) kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Uwekezaji na Uendelezaji wa Biashara wa Angola yamesainiwa, hatua inayotarajiwa kuongeza uwekezaji na kuimarisha sekta za kilimo, utalii, nishati, na madini.

Kwa upande wa usalama wa kikanda, Rais Samia amesifu juhudi za Rais Lourenço katika utatuzi wa migogoro barani Afrika na kuahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Angola katika kuimarisha amani na usalama wa bara hilo.

 

Send this to a friend