Katika mkakati wa kupunguza kero ya foleni jijini Dar es Salaam, Serikali inafanya mazungumzo na kampuni ya China Overseas Engineering Group Co. Ltd. (COVEC) ambayo imeonesha nia kuwekeza Dola za Marekani bilioni 1 (TZS trilioni 2.7) kujenga barabara ili kupunguza kero ya foleni mkoani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), David Kafulila, amesema mwekezaji huyo tayari amefanya kazi za awali, kama vile upembuzi yakinifu na uchambuzi wa kiuchumi, na sasa inataka kuingia katika Hati ya Makubaliano na Serikali ili iweze kufanya upembuzi yakinifu kamili ya mradi huo.
“Utafiti uliofanywa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) mwaka 2020 umebaini kuwa biashara hupoteza asilimia 20 za faida zao kutokana na foleni za magari kwenye barabara za Dar es Salaam,” amesema Kafulila.
Kwa mujibu wa Kafulila, kampuni ya COVEC inataka kujenga barabara 10 za mazunguko (ring roads) ikiwa ni pamoja na barabara 6 za ndani (inner ring roads) na barabara 4 za nje (outer ring roads).
Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kunatarajiwa kupunguza foleni kwenye barabara kuu za Dar es Salaam, kwani magari yataweza kutumia barabara za kuzunguka ambazo zitalipiwa (toll roads).