Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Guinea-Bissau zimejadiliana kuhusu ushirikiano katika kukuza uchumi wa bluu na kilimo cha korosho hususani katika kuongeza utafiti na kuliongezea thamani zao hilo ambalo linalimwa katika nchi zote mbili.
Akizungumza leo na waandishi wa Habari mara baada ya kumpokea Rais wa Guinea-Bissau Ikulu Dar es Salaam, ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku tatu, amesema nchi hizo pia zitashirikiana katika kukuza maeneo huru ya biashara na uwekezaji.
“Tumezungumza mambo mengi yenye lengo la kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili. Tulijikita zaidi kwenye nyanja za kiuchumi, pia tumebadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya kikanda na kimataifa ikiwemo ukuzaji wa amani na usalama barani Afrika,” amesema.
Aidha, amesema bara la Afrika liko mbioni kuhakikisha Eneo Huru la Biashara Afrika linafunguka, lengo likiwa kukuza zaidi kiwango cha biashara kati ya nchi za Afrika, ambapo pia kuanzishwa kwa soko hilo kutachochea ukuaji wa viwanda, uingizaji wa thamani wa mazao pamoja na kuleta ajira kwa vijana.