Tanzania na India kuongeza matumizi ya fedha za ndani katika biashara

0
33

Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi wamekubaliana kuongeza matumizi ya fedha za nchi badala ya fedha za kigeni katika biashara kati ya nchi hizo mbili.

Hatua hiyo inalenga kupunguza matumizi ya dola za Marekani na badala yake kutumia fedha za ndani, ambayo inatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa Tanzania na India.

Kulingana na takwimu za India za mwaka 2022/23, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili imefikia dola bilioni 6.7 [zaidi ya TZS trilioni 14], ambayo ni ongezeko kubwa kutoka dola bilioni 3.1 mwaka 2021/22 kwa mujibu wa takwimu za Tanzania. Hii inaonyesha ukuaji mkubwa wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo yao, Waziri Mkuu Modi alielezea lengo la hatua hiyo ni kuongeza biashara na wakati huo huo kupunguza gharama za biashara kwa kutumia fedha za ndani.

India na Tanzania sasa zimebadili uhusiano wao kutoka ule wa kawaida wa kidiplomasia kuwa wa kimkakati ambapo nchi hizo zimechagua maeneo mahususi zitakazoshirikiana katika masuala ya kimkakati ambayo yana maslahi kwa pande zote mbili.

Mazungumzo ya kuwezesha biashara kwa kutumia fedha za ndani kama Shilingi ya Tanzania na Rupia ya India, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika huduma za afya na ulinzi, sasa yatakuwa rahisi zaidi kufanikisha kutokana na hatua hiyo.

Hii ni ushindi mkubwa kwa diplomasia ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwani imefanikisha makubaliano haya ambayo yanazilenga nchi tajiri na zenye ushawishi mkubwa duniani.

Send this to a friend