Tanzania na Kenya kuondoa vikwazo vya kibiashara vilivyobaki

0
23

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Kenya zimekubaliana kufanyia kazi vikwazo vya kibiashara vilivyopo kati ya nchi hizo mbili ili kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wa kibiashara.

Akizungumza leo pamoja na Rais wa Kenya, William Ruto na vyombo vya habari Oktoba 10, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam, amesema baada ya wataalam kutoka pande zote mbili kufanya tafiti walibaini kuwepo kwa vikwazo 68 ambapo vikwazo 54 visivyo vya kikodi viliondolewa na kubaki vikwazo 14.

Aidha, Rais Samia amesema katika mazungumzo yake na Rais wa Kenya, Wiliam Ruto wamekubaliana kuimarisha mpaka wa kimataifa kati ya Kenya na Tanzania pamoja na kushirikiana kudhibiti vitendo vya kiuhalifu na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa ukaribu ili kuangalia namna ya kidhibiti uhalifu unaofanywa.

“Tumetaka wakae waangalie kwa nchi zetu hizi mbili tutayafanya vipi kwa sababu tumekuwa tunapata sifa mbaya ya usafirishaji watu wakati wanaosafirishwa siyo Watanzania, sisi tunakamata tu lakini wakifika kwetu rekodi za dunia wanaiona Tanzania au Kenya,” amesema.

Aidha, kwa upande wa Rais Ruto amesema nchi ya Kenya inataka kufanya kazi na kushirikiana na Tanzania pamoja na kuhakikisha kuwa nchi hizo mbili zinakua ikiwa ni pamoja na kugawana utajiri na fursa zilizopo.

“Ile historia ya zamani, ya kidogo mabishano tumeyaweka nyuma yetu, tunataka kujenga uhusiano ambao una manufaa pande zote. Tunataka Watanzania wafaidike, tunataka Wakenya wafaidike kwasababu Wakenya wakifaidika ni ndugu zao Watanzania wamefaidika ,vilevile ndugu zetu Watanzania wakifaidika na sisi pia kama Wakenya tutafaidika,”ameeleza.