Tanzania na Malawi zakubaliana kumaliza changamoto za kibiashara

0
42

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Malawi zinahitaji kushughulikia changamoto za kibiashara zilizopo ili kutoa urahisi wa nchi hizo kufanya kazi kwa pamoja na kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Ameyasema hayo leo Julai 06, 20223 katika sherehe ya maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Malawi zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa wa Bingu, Lilongwe nchini humo.

“Bahati nzuri suala hili lilijadiliwa katika tume ya pamoja kati ya nchi zetu mbili mwaka jana, na naambiwa kuwa majadiliano yalikuwa ya kirafiki katika kukubaliana baina ya pande zetu zote mbili kufanya kazi kwa pamoja katika kutatua changamoto,” amesema.

Amesema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo na Malawi  pamoja na kuiunga mkono katika kukuza uchumi wa nchi hiyo kwa kuwa uchumi wake ukikua ni sawa na uchumi wa Tanzania umekua pia.

“Tanzania inaridhishwa na uhusiano wa hali ya juu uliopo kati ya nchi zetu mbili, ahadi yetu kwa Malawi ni kuhakikisha uhusiano huu unakua kutoka kiwango hadi kiwango,” amesema.

Akizungumzia uhuru wa miaka 59 ya nchi hiyo, Rais Samia ameipongeza Malawi kwa kudumisha amani, umoja na ushirikiano na kueleza kuwa uhuru wa nchi hiyo umeifanya Tanzania kupata rafiki, jirani wa kutegemea na mshirika wa kiuchumi.

Send this to a friend