Tanzania na Msumbiji zasaini makubaliano ya kuimarisha ushirikiano

0
0

Rais Samia Suluhu Hassan amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo ushirikiano wa dhati baina ya nchi hizo mbili katika kufikia malengo ya maendeleo.

Ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Rais Daniel Chapo kuwasili Ikulu, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Kiserikali kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika kikao cha pamoja kilichofanyika baina viongozi hao, Rais Samia amesema wamejadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ikiwemo kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kufanya kazi kwa urahisi, kuharakisha uanzishwaji wa vituo vya pamoja vya biashara mipakani na kuanzisha tume ya pamoja ya kiuchumi.

Kwa upande wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, viongozi hao wamekubaliana kuendeleza ujenzi wa barabara zilizoko mipakani zinazounganisha nchi hizo, kufanya mapitio ya mkataba wa ushirikiano wa usafiri wa anga, na kuimarisha usafiri wa baharini kupitia Ziwa Nyasa na Mto Ruvuma.

Vilevile, viongozi hao wamejadili umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja, kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya rasilimali za baharini, na kufanya kazi kwa ukaribu kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu, utalii na usafirishaji.

Kwa upande wa kilimo, Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuimarisha uhusiano kwenye sekta ya kilimo ikiwemo kubadilishana uzoefu na kufanya tafiti za pamoja hususani kwenye zao la korosho.

Serikali yasisitiza hakuna sheria iliyokiukwa katika utekelezaji wa majukumu yake

Mbali na hayo, nchi hizi zimekubaliana kushirikiana kwenye sekta ya mawasiliano, madini, elimu na afya na masuala ya kimataifa, ambapo zimejadili kushirikiana katika majukwaa ya kikanda kupitia SADC, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.

Rais Samia ameongeza kuwa katika mazungumzo yao wamejadili juu ya masuala ya amani na usalama wa bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na kukubaliana kufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na uhalifu wa kimataifa ukiwemo ugaidi na ujangili.

Kwa upande wake Rais wa Msumbiji, amesema baada ya majadiliano hayo, Tanzania na Msumbiji zimesaini mikataba mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo kubadilishana wanafunzi wa elimu ya juu, mkataba wa kuanzisha kituo cha pamoja mpakani, mkataba wa kubadilishana wafungwa, na makubaliano kati ya redio ya Msumbiji na Shirika la Utangazaji Tanzania.

Send this to a friend