Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kuchochea zaidi utalii pamoja na biashara baina ya Tanzania na Poland, ameelekeza kuchukuliwa kwa hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za ndege moja kwa moja kutoka Poland kuja Tanzania.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Poland, Andrzej Duda, Ikulu jijini Dar es Salaam, ambapo amebainisha kuwa Poland ni miongoni wa nchi 10 ambazo raia wake hutembelea kwa wingi Tanzania kwa ajili ya utalii.
“Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, watalii 6,000 kutoka Poland walitembelea nchi yetu. Ili kuchochea zaidi utalii pamoja na biashara, tumewaelekeza wataalamu wetu kuchukua hatua zitakazowezesha kuanza kwa safari za ndege moja kwa moja kutoka Poland kuja Tanzania, na tumeweka ombi letu hilo kwa msisitizo mkubwa kwa wenzetu wa Poland,” amesema Rais Samia.
Aidha, katika ziara ya Rais Duda nchini, Rais Samia amesema Tanzania na Poland zimekubaliana kuhamasisha uwekezaji katika maeneo ya kimkakati ikiwemo viwanda, uzalishaji, nishati, madini, gesi asilia na uchumi wa bluu. Pia zimejadiliana kushirikiana katika nyanja za elimu, kilimo, biashara, uwekezaji, utalii na TEHAMA.
Kwa upande wake Rais Duda ambaye yuko nchini kwa ziara ya siku mbili, amesema anaamini kuwa uwekezaji kutoka kwa wajasiriamali na wawekezaji kutoka nchini Poland utaongezeka kwa wingi nchini Tanzania kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la viwanda.
Mbali na hayo, Rais Duda amemualika Rais Samia kutembelea nchini Poland kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.