Tanzania na Romania zakubaliana kukuza biashara

0
51

Rais Samia Suluhu Hassan amesema moja kati ya mambo waliyojadiliana na Rais wa Romania, Klaus Iohannis ni kuimarisha biashara kati ya mataifa hayo mawili ambapo wafanyabiashara wa Tanzania waende nchini Romania na wale wa Romania waje Tanzania kujifunza na kufanya biashara kwa pamoja.

Akizungumza Novemba 17, 2023 mara baada ya majadiliano na Rais huyo Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia amesema lengo la wafanyabiashara wa nchi hizo mbili kukutana ni kubadilishana uzoefu ili kukuza biashara zao pamoja na kuongeza uwekezaji.

Aidha, Tanzania na Romania zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, usalama wa chakula, kukabiliana na majanga pamoja na elimu ambapo nchi hiyo imetoa nafasi 10 za ufadhili kwa ajili ya Watanzania kusoma nchini humo, huku Tanzania ikitoa nafasi tano kwa wanafunzi wa Romania kuja kusoma nchini.

Denmark yasitisha mpango wa kufunga ubalozi wake nchini

“Romania imekuwa mbia wetu kama nchi na pia kama nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya, hivyo ni dhamira yetu kuendelea kuimarisha uhusiano huu,” amesema Rais Samia.

Mbali na hayo, Rais Samia amepongeza azma ya serikali ya Romania kuimarisha uhusiano na nchi za Afrika ikiwa ni kiashiria kingine cha umuhimu wa bara la Afrika katika ulingo wa kimataifa.

Naye, Rais Klaus Iohannis amesema Tanzania inaweza kuitegemea Romania kama mshirika watakaoweza kusaidia katika kujenga mahusiano mazuri na nchi za Umoja wa Ulaya.

Send this to a friend