Tanzania na Rwanda kwa pamoja zimeafikiana kuweka mazingira mazuri ambayo yatasaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kama moja ya njia za kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.), alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali, Rwanda pamoja na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dkt. Vincent Biruta.
Rwanda imeongeza matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 80 kwa usafirishaji wa mizigo yake.
Mbali na usafirishaji, Makamba na Biruta walijadili masuala mengine muhimu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na nishati, kilimo na teknolojia.
Nchi 10 za Afrika zenye idadi kubwa ya wanawake Serikalini
Mbali na hayo, Makamba ametembelea Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari Kigali (Kigali Genocide Memorial) na kuweka taji la maua katika kaburi ambapo takribani miili ya watu 2500 waliopoteza maisha katika Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994 imezikwa.
Waziri Makamba amewasihi wale wote wenye ushawishi mkubwa na nia njema ama ovu kwa nchi zao kutembelea makumbusho hiyo ili kujifunza umuhimu wa umoja na athari chanya ama hasi zinazoweza kuletwa na matendo yao kwa miaka ya mbeleni.