
Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika matumizi ya bandari, biashara ya gesi asilia na mafuta safi kutoka Uganda pamoja na miradi ya reli ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwa nchi zisizo na bandari.
Akizungumza leo Februari 07, 2026, Ikulu Dar es Salaam baada ya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais Samia amesema Uganda ni miongoni mwa nchi zinazotegemea bandari za Tanzania, hususan Dar es Salaam na Tanga, kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo.
“Nchi zetu ambazo hazina bandari zinategemea sana bandari zetu hususan Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Kwa Uganda wanategemea bandari ya Dar es Salaam na Tanga, tumezungumza namna ya kupata nafasi ya kuizitumia bandari hizi na kusafirisha mizigo,” alisema Rais Samia.
Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 ina mpango wa kujenga reli itakayounganisha Tanga hadi Musoma, mradi utakaorahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda Uganda kupitia Ziwa Victoria.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kuchukua hatua za pamoja kuondoa vikwazo vya biashara pamoja na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kukuza uchumi na biashara ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.
“Jambo lingine tulilozungumza ni kuondosha vikwazo vya biashara. Kila tunapoondosha vikwazo hivyo, iwe vya ushuru wa kikodi au visivyo vya kikodi, biashara zinakua,” ameeleza.
Rais Museveni amezuru Tanzania kwa ziara ya kikazi ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.








