Tanzania na Uganda zathibitisha dhamira ya kuendeleza ushirikiano

0
1

Tanzania na Uganda zimethibitisha tena dhamira yao ya kuimarisha ushirikiano wa uwili, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya pamoja, na kuibua maeneo mapya ya ushrikiano.

Akifungua  kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kinachofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa idara ya afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ali Bujiku amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uganda katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Balozi Bujiku ameeleza kuwa mkutano huo ni fursa kwa wataalamu wa pande zote  kufanya tathmini ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika JPC ya nne mwaka 2022, kujadili changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, na kupendekeza njia bora za kuimarisha ushirikiano huo.

“Mjadala wetu leo unaakisi upeo mpana na wa kimkakati wa ushirikiano wetu. Tutajadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, uhamiaji, kilimo, afya, elimu, utamaduni pamoja na biashara.


“Sekta hizi ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa watu kwa watu na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya pamoja,” amesema Balozi Bujiku

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kushughulikia vikwazo vya biashara vinavyoathiri mtiririko wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili. Amebainisha kuwa kuondoa vikwazo hivyo kutasaidia kufungua fursa kubwa za kiuchumi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na watu.

Balozi Bujiku pia aligusia umuhimu wa kuboresha miundombinu ya mawasiliano na usafirishaji kati ya Tanzania na Uganda, akitaja miradi ya kimkakati ya kikanda ikiwemo bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki pamoja na barabara na miundombinu mingine ya usafiri ambayo inalenga kuongeza ufanisi wa biashara na kuimarisha ujumuishaji wa kikanda.

Kwa upande wake, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Kanali Mstaafu Fred Mwesigye amesisitiza umuhimu wa kutatua changamoto zilizopo na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, pia ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kuonesha uongozi madhubuti katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na kuteuliwa kwa Mtanzania Balozi Patrick Mbundi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo.

Send this to a friend