Tanzania ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Afrika

0
94

Tanzania inashika nafasi ya pili barani Afrika kwa uzalishaji wa tumbaku baada ya Zimbabwe ambapo kwa mwaka huu wa 2024 imezalisha tani 122,000 za tumbaku kutoka tani 65,000 mwaka 2021.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati Rais Samia Suluhu Hassan akiweka Jiwe la Msingi kwenye ujenz wa Kiwanda cha Sigara cha Serengeti (SCC) na upanuzi wa Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku (MTPL) ikiwa ni sehemu ya Ziara yake mkoani Morogoro.

Katika hotuba hiyo, Bashe amesema mauzo ya tumbaku nje ya nchi yameongezeka na kufikia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 400 [sawa na TZS trilioni 1.07] ambapo isingekuwa mvua za El nino zilizoathiri mazao, Tanzania ingekuwa nafasi ya kwanza Afrika kwa uzalishaji.

“Tulijiwekea lengo la kuzalisha tani 200,000 lakini tumezalisha tani 122,000. Lakini Mheshimiwa Rais, maamuzi uliyoyachukua, bei ya tumbaku imeongeza kutoka wastani wa Dola 1.3 mpaka Dola 2.4,” amesema.

Waziri Bashe amesema mafanikio hayo yanachangiwa na jitihada za Rais Samia Suluhu kukutana na wadau na wanunuzi mbalimbali wa tumbaku duniani.

Send this to a friend