Tanzania ya viwanda inavyohitaji mazingira bora kukuza ubunifu wa kiteknolojia

0
37

Wiki jana tumeona ufunguzi wa maonyesho katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya. Tukio hilo muhimu lilileta pamoja wanafunzi na waalimu wa vyuo na taasisi mbalimbali za mkoa wa Mbeya kuonyesha na kujadili fursa zitokanazo na ubunifu wa kiteknolojia. 

Katika hotuba yake, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi na Elimu ya Ufundi chuoni hapo Dkt John John aliisihi Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini (COSTECH) kutengeneza mfuko wa fedha kutambua na kusaidia vyuo na wanafunzi katika tafiti na maendeleo. Dkt John aliongeza kuwa mfuko wa kusaidia wa namna hiyo utasaidia kukuza ubunifu wa kibiashara katika teknolojia na utanufaisha taifa katika lengo lake la kuwa na uchumi wa viwanda, jambo ambalo sote tunafahamu kuwa ni lengo kubwa la Rais Dkt Magufuli. 

Kutokana na kukweli huu, ni vyema basi tukajadili na kutafakari namna gani kama taifa tunaweza kuwa na mipango inayokuza ubunifu katika teknolojia ili kusukuma mbele kasi ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.Hatuhitaji kutazama mbali sana kuona matunda ya uchumi bunifu katika zama hizi za teknolojia. Tazama kwa mfano sekta ya mawasiliano ya simu namna ambavyo imekua si tu kwa ajili ya kupiga/kupokea simu na kutuma meseji. Leo hii simu si tu ya kupiga na kutuma meseji, bali simu sasa inatuma fedha, inaperuzi mtandao, inatusaidia kupata huduma za afya, na kadhalika. Sekta nyingi zinaweza kutazama sekta ya mawasiliano ya simu na kujifunza kuhusu ubunifu. Mazingira bora ya biashara ni msingi wa kujenga ubunifu wa kiteknolojia ambao leo tunauona na kufaidika na matunda yake katika sekta ya mawasiliano ya simu. Bahati nzuri, sera ya kujenga mazingira bora na endelevu ya biashara imo katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa serikali.

Ubunifu katika teknolojia ambao tunauhitaji ili kujenga Tanzania ya viwanda kama ambavyo tumeuona kwenye sekta ya mawasiliano ya simu utawezekana kama tukiendelea kujenga mazingira rafiki ya kufanya biashara na kuunga mkono uwekezaji toka sekta binafsi.

Send this to a friend