Tanzania yachaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawasiliano Duniani
Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Shirika la Mawasiliano Duniani (International Telecommunication Union – ITU) kwa mwaka 2023 hadi 2026, ikiwa ni miongoni mwa nchi 13 zinazowakilisha Bara la Afrika.
Baraza la ITU ni chombo cha Shirika la Mawasiliano Duniani chenye mamlaka ya kusimamia masuala ya kisera ya mawasiliano ya simu ili kuhakikisha kuwa shughuli za ITU, sera na mikakati inasimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia mazingira ya mawasiliano leo yanayobadilika kwa kasi.
Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amethibitisha dhamira ya Tanzania katika ITU kwa miaka 4 itakayokuwa katika baraza hilo.
“Napenda kusisitiza kuwa Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi nyingine wanachama, Sekretarieti ya ITU na ofisi za Kanda ili kuifanya ITU kuwa chombo muhimu cha kimataifa ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya nchi zote wanachama kama mjumbe wa Baraza la ITU” alisema Mhe.Nnauye.
Kuanzia Januari 1, 2023, viongozi watano waliochaguliwa pamoja na Wajumbe 48 wa Baraza la ITU wataanza uongozi wa miaka minne hadi 2026.