Tanzania yaeleza ilivyoathiriwa na vita ya Urusi na Ukraine

0
41

Tanzania imesema ilipiga kura ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine, kwani inasisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ametoa ufafanuzi huo na kuongeza kuwa Sera ya Tanzania kuhusu namna ya kutatua changamoto za migogoro inapojitokeza ni kwa kutumia njia za kidiplomasia.

Tanzania imesema msimamo wake katika mgogoro kati ya Urusi na Ukraine ni pande zote kutafuta suluhu kwenye meza ya mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula amesema hayo akifanya mahojiano na chombo cha habari kutoka China. pic.twitter.com/zjFFJb49zo

Balozi Mulamula amesisitiza kuwa Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijabadilika tangu uhuru na kuwa Tanzania inaamini hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika hasa panapokuwepo na utashi na nia njema ya kumaliza mgogoro na kwamba njia ya kidiplomasia ndio chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro kati ya Urusi na Ukraine.

“Sisi msimamo wetu na Sera yetu na msingi wetu wa Sera yetu ya Mambo ya Nje ni kutofungamana na pande zozote, hivyo kutokupiga kura ni kuonesha msimamo wa Tanzania,” amesema Balozi Mulamula

Ameongeza kwamba Tanzania imeathirika na mgogoro huo ikiwemo baadhi ya wanafunzi wa kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Urusi kukatisha masomo yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika pamoja na ongezeko la bei ya petroli na gesi duniani.

Kutokana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi Tanzania ililazimika kuwaondoa raia wake nchini Ukraine hususani wanafunzi takribani 300 waliokuwa wakisomea masuala ya udaktari nchini humo.

Send this to a friend