Tanzania yafikia makubaliano kuanza uchimbaji wa gesi asilia (LNG) Lindi

0
48

Baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kampuni za uchimbaji wa mafuta na gesi za Equinor, Shell pamoja na Exxon Mobil, hatimaye serikali ya Tanzania imefikia makubaliano na kampuni hizo siku ya Ijumaa ya Mei 19, 2023 kwa ajili ya uchimbaji wa gesi asilia (LNG) mkoani Lindi nchini Tanzania.

Kufikiwa kwa mkataba huu ni hatua muhimu kwa mradi uliocheleweshwa kwa muda mrefu, ambapo utafungua fursa nyingi na kubwa pwani ya Tanzania. Mkataba kati ya Tanzania na kampuni hizo, unajumuisha vipengele vikuu vya makubaliano ya serikali mwenyeji kwa kutoa mfumo wa udhibiti na makubaliano ya kugawana uzalishaji, ukaguzi na mapitio ya kisheria na uhakikisho wa ubora kabla ya kutiwa saini ndani ya wiki chache zijazo, alisema mwakilishi wa Equinor kutoka Norway.

“Makubaliano haya ya kuanza mchakato wa kuchimba gesi asilia (LNG) ni hatua muhimu ya kufikia fursa kubwa za kimaendeleo kwa Tanzania na dunia kwa ujumla”, alisema mwakilishi mkaazi wa kampuni ya Equinor Bwana Unni Fjaer.

TPA yakanusha madai ya urasimu Bandari ya Dar es Salaam

Mkataba huo pia unahusisha matumizi ya ardhi na usalama, alisema mwendesha mazungumzo mkuu wa Tanzania, Charles Sangweni. “Tunafurahi ni hatua kubwa kuelekea utekelezaji wa mradi ingawa bado tuna mengi ya kufanya. Ikiwa kila kitu kitakwenda vizuri kama ilivyopangwa, nina imani uamuzi wa uwekezaji wa mwisho utafikiwa mwaka 2025,” Sangweni alisema.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Linkedin, Mwenyekiti wa Shell Tanzania Jared Kuehl, alisema kwamba hatua ya kimkataba inayofuata itahusisha hatua za kihandisi za kuunda mpango kazi wa utekelezaji wa mradi huo.

Equinor na Shell ni waendeshaji wenza wa mradi huu mkubwa wa mafuta na gesi asilia (LNG), wakati kampuni ya Exxon, Pavilion Energy, Medco Energi, na kampuni ya mafuta ya taifa ya Tanzania TPDC ni washirika.

Tanzania ilisema mwaka 2014 kuwa mradi huo unaweza kugharimu dola bilioni 30 (TZS trilioni 70), lakini wachambuzi wamesema kuongezeka kwa gharama za maisha katika miaka ya hivi karibuni kunaweza kuongeza mabilioni ya fedha zaidi kwenye uwekezaji wa mradi huo.

Kampuni ya Shell inamiliki kitalu namba 1 na 4 vya gesi nchini Tanzania, ambavyo vyote vina takriban futi za ujazo trilioni 16 za gesi. Huku ya Kampuni ya mafuta na gesi ya Norway, Equinor, ikimiliki kitalu namba 2 ikiwa ni mshirika na ExxonMobil yenye hisa katika kitalu hicho kinachokadiriwa kuwa na gesi yenye futi za ujazo trilioni zaidi ya 20.

Send this to a friend