Tanzania yafuzu Kombe la Dunia (Wenye Ulemavu)

0
71

Timu ya Soka ya Tanzania ya Wenye Ulemavu, Tembo Warriors imefuzu kushiriki Mashindano ya Dunia ya mchezo huo yatakayofanyika nchini Uturuki 2022.

Tembo Warriors imefuzu baada ya kuifunga timu ya Cameroon mabao 5-0 katika mchezo wa nusu fainali ya Soka ya Bara la Afrika kwa Wenye Ulemavu (CANAF 2021) yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.

Katika mechi zote za mashindano hayo Tanzania imepoteza mechi moja tu ya Uganda mbayo ilifungwa goli 1-0, ambapo Tembo iliifunga timu ya Morocco 2-1 na Sierra Leone goli 1-0.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mechi hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewahakikishia kwamba Serikali itaendelea kuisaidia timu hiyo ili iendelee kufanya vizuri maandalizi ya Kombe la Dunia.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema kwa kuwa safari ya kuelekea kombe la dunia imekamilika kazi iliyobaki ni kuhakikisha kuwa kombe la Afrika linabaki Tanzania.

Magoli ya Tanzania yamefungwa na Alfan Kyanga dakika ya 2 na 15 , Ramadhan Chomole dakika ya 18, na Frank Ngailo dakika ya 36 na 44.

 

Send this to a friend