Tanzania yajiunga rasmi COVAX, yaahidiwa chanjo kutoka Umoja wa Ulaya

0
38

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania tayari imejiunga na mpango wa kimataifa wa ugawaji wa chanjo ya #COVID19 kwa nchi masikini (COVAX facility).

Rais amesema hilo wakati akizungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel na kuongeza kuwa Tanzania itawasilisha mahitaji yake kwa EU ili kupata msaada.

Michel amempongeza Rais Samia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona. Vilevile amemueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

Kwa upande wake Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hususani matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Send this to a friend