Tanzania yakanusha kuruhusu kilimo na matumizi ya bangi

0
82

Serikali imesema kuwa haijaruhusu matumizi na kilimo cha bangi, na hivyo kuwataka wananchi kujikita katika kilimo cha mazao mengine yenye tija.

Msimamo huo umetolewa na Gerald Kusaya, ambaye ni Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) jijini Dodoma kuelekea katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya Juni 26 itakayofanyika kitaifa jijini humo.

“Sheria yetu mama bado iko pale pale haijaruhusu kilimo cha bangi wala matumizi ya bangi hapa nchini,” amesema Kusaya.

Ameongeza kuwa, kwa sababu hakuna mabadiliko yoyote ya sheria, hategemei kuona watu wakifanya kilimo au kutumia bangi.

Kuhusu mataifa yaliyoruhusu kilimo cha bangi, Kusaya amesema, “ni lazima mfahamu kuna aina zaidi ya 20 za bangi, kwa hiyo inategemea hayo mataifa ni aina gani ya bangi imeruhusiwa.”

Akitoa taarifa yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kuwa bangi imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayotumika zaidi duniani ambapo kwa mwaka 2018 ilitumiwa na watu takribani milioni 192.

Kwa mujibu wa DCEA, madhara ya matumizi ya bangi ni pamoja na kuamsha magonjwa ya akili, kuona na kusikia vitu tofauti ja uhalisia, uhalifu, utegemezi, saratani ya mapafu, kupunguza kumbukumbu na kuchochea matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimeruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi ni Lesotho, Zambia na Zimbabwe, ikiwa ni njiabya kukuza biashara kimataifa kutokana na uhitaji wa bangi katika shughuli za kitabibu na kujiburudisha.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni, “Tuelimishane Juu ya Tatizo la Dawa za Kulevya Kuokoa Maisha”

Send this to a friend