
Serikali ya Tanzania imekanusha madai yaliyotolewa na wanaharakati wa Kenya na Uganda, Boniface Mwangi na Agather Atuhaire kuhusu kufanyiwa unyanyasaji wa kingono baada ya kushikiliwa nchini.
Akizungumza kwenye mahojiano na DW Kiswahili, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema madai hayo yaliyotolewa hayana ukweli na yana nia ya kuichafua Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Hii nchi ina heshima zake, inaheshimiwa na kila mtu na watu wote wanaifahamu Tanzania, wao si watu wa kwanza kuja Tanzania, watu wengi wamekuja Tanzania. Kama wao wanakwenda kuzalisha tuhuma zao za uongo, wacha waendelee kufanya lakini Tanzania haiko hivyo. Wao walivunja sheria, wamechukuliwa hatua,” amesema.
Ameongeza kuwa “hii nchi ina taratibu zake ina utamaduni wake, ina amani yake. Aina ya siasa tunayofanya Tanzania ni utamaduni wa siasa ya Tanzania, mtu asitoke huko akalazimisha utamaduni wa nchi yake akataka kuuleta Tanzania.”
Aidha, amesema uhusiano wa Tanzania na Kenya hauwezi kuharibiwa na watu wachache wenye nia ovu, kwani Tanzania na Kenya ni ndugu.
