Tanzania yalegeza masharti ya safari za ndege nchini

0
26

Serikali ya Tanzania imelegeza vizuizi vya safari za ndege kuja na kutoka nchini ambapo sasa baadhi ya makundi ya safari yataruhusiwa kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.

Safari za ndege ambazo zitaruhusiwa ni pamoja na zile za ndege zinazochukua raia wa kigeni kuwarejesha kwenye nchi zao, ndege za misaada ya kibinadamu na misaada ya kitabibu, ndege zinazotua kwa dharura ambapo abiria hawatoruhusiwa kutoka ndani ya ndege.

Mwezi mmoja uliopita Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilisitisha safari za ndege za abiria kutoka na kuingia Tanzania ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari amesema kuwa wamepokea maombi mengi ya ndege kuja kuchukua raia wakigeni, ndio sababu wamelegeza masharti ya safari za ndege.

Lakini ameongeza kuwa ndege hizo zitakapofika nchini baada ya kupata kibali, wahudumu wa ndege hawatoruhusiwa kutoka ndani ya ndege.

Hadi Mei 8 mwaka huu nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, Lebanon, Pakistan, Uturuki na Ethiopia zilikuwa zimefanikiwa kuwarejesha makwao raia wake waliokuwa wamekwama Tanzania.

Send this to a friend