Tanzania yalitaarifu Shirika la Afya Duniani kuhusu kupungua kwa wagonjwa wa Covid-19

0
21

Tanzania imelieleza Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu mafanikio iliyoyapata kutokana na hatua ilizochukua kukabiliana na virusi vya corona, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kasi kwa maambukizi na idadi ya wagonjwa wa Covid-19 nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi alipofanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus.

Pia, Prof. Kabudi amemueleza Dkt. Ghebreyesus kuhusu uamuzi wa serikali wa kuruhusu shughuli za michezo, kufungua vyuo, pamoja na msimamo wa serikali kutoingilia shughuli za kidini.

Kabudi amesisitiza kuwa, serikali ya Tanzania ipo tayari kuendelea kushirikiana na kujadiliana na wadau wote wa katika kuongeza nguvu na mbinu za kukabiliana na maambukizi ya Covid-19.

Kwa upande wake kiongozi wa shirika hilo lenye dhamana ya kusimamia afya za watu duniani amesema kuwa anatambua jitihada zilizochukuliwa na Tanzania na litaendelea kutoa ushirikiano hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Corona.

Kwa miaka 57 sasa shirika hilo limekuwa likifanya kazi zake nchini Tanzania katika kutekeleza miradi na programu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa misaada ya kitaalamu, mafunzo na vifaa.

Send this to a friend