
Wizara ya Kilimo imetangaza kuondoa mazuio yote yaliyowekwa kwa nchi za Afrika Kusini na Malawi ya kuingiza mazao nchini kufuatia majadiliano yanayoendelea kutatua suala hilo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara imesema Serikali za Malawi na Afrika Kusini zimewasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Kilimo ili kutafuta suluhisho.
“Makubaliano yaliyofikiwa ni kwamba Serikali ya Malawi itatuma ujumbe wake Mei 02, 2025, utakaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje akiambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo ili kukutana na ujumbe wa Tanzania jijini Dodoma chini ya uratibu wa Waziri wetu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” imesema taarifa.
Aidha, Serikali imewahakikishia wakulima na wananchi uhuru wa biashara ya mazao ya kilimo kulingana na matakwa ya afya ya mimea, rasilimali za nchi zilizopo na mahusiano mapana ya kidiplomasia kwa faida ya wote.