Tanzania yapanda viwango vya tathmini ya uchumi duniani

0
39

Kampuni ya Moody’s Investors Service ambao ni wabobezi katika masuala ya kupima uhimilivu wa deni duniani imeipandisha Tanzania kwa daraja moja juu zaidi hadi B1 (imara) kutoka B2 (chanya), matokeo yaliyochangiwa na ukuaji imara wa Pato la Taifa kunakotokana na uchumi thabiti na uwekezaji mkubwa wa sekta binafsi.

Aidha, ripoti hiyo inaashiria kustawi kwa uchumi wa Tanzania hivyo kuimarisha imani kwa mashirika ya fedha ya kimataifa kuwa nchi hiyo inaweza kumudu kulipa madeni yake kwa wakati.

“Uboreshaji hadi B1 unaonyesha rekodi ya Tanzania ya ustahimilivu wa uchumi wa Tanzania katika changamoto za kiuchumi duniani kama vile janga la UVIKO19, mfumuko wa bei na vita,” Moody’s imesema katika taarifa yake.

Ukuaji halisi wa Pato la Taifa wa Tanzania ulikuwa wastani wa asilimia 6 kuanzia mwaka 2015 hadi 2022, ukiimarishwa na ukuaji katika sekta mbalimbali kama kilimo, utalii, uchimbaji madini, na ujenzi.

Tanzania yapokea trilioni 1.4 kukabiliana na Malaria, TB na UKIMWI

Moody’s imesema kasi ya mageuzi inazidi kuimarika nchini Tanzania na mamlaka zimechukua hatua madhubuti kuboresha nguvu za kitaasisi na kuimarisha mazingira ya biashara.

Moody’s imebaini mabadiliko chanya katika mwelekeo wa Tanzania chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan ikitarajia Pato la Taifa kuwa imara katika siku za usoni.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa uchumi wa Tanzania umepata daraja la juu zaidi kushinda nchini nyingine za Afrika Mashariki zikiwemo Kenya (B3 hasi), Uganda (B2 hasi) na Rwanda (B2 imara).

Send this to a friend