Tanzania yapeleka madaktari bingwa wa moyo Zambia

0
41

Serikali imetuma madaktari bingwa 12 kwenda nchini Zambia kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa watoto ikiwa ni sehemu ya kuendelea kutanua wigo wa tiba utalii na kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Wataalamu hao kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCI) ambao watakaa nchini humo kwa wiki mbili wanatarajiwa kutoa matibabu ya upasuaji mkubwa wa magonjwa ya moyo hususani kwa watoto chini ya miaka 15 na kuisaidia nchi ya Zambia kuanzisha huduma ya matibabu ya moyo nchini humo.

Hayo yamebainishwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akizungumza na vyombo vya habari juu ya huduma za mkoba (outreach services) za matibabu ya kibingwa nje ya Tanzania kutoka JKCI.

“Lengo la Tanzania kuwa na madaktari bingwa na miundombinu ya kutoa huduma za kibingwa na bingwa bobezi ni kuhakikisha fedha ya kigeni haiendi nje ya nchi ili kusaidia kugharamia watanzania wasio kuwa na uwezo wa kupata matibabu hapa nchini,” ameeleza Dkt. Mollel.

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Dkt. Peter Kisenge amesema madaktari hao watafanya upasuaji kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 na wanatarajia kufanya upasuaji kwa watoto 10.

“Mpaka sasa Zambia washapokea wagonjwa 15 wanaohitaji huduma ya upasuaji wa moyo, hivyo watalaalamu wetu watatoa Huduma kwa hao wagonjwa na wengine watakao hitajika kupata huduma zaidi watapewa rufaa ya kuja nchini kupata matibabu zaidi”, amesema.

Send this to a friend